Idadi kubwa ya wafugaji hupenda kuwekeza katika ufugaji kuku, aidha kuku wa kienyeji au wa kisasa yaani wa mayai au nyama. Hujenga mabanda, hununua vyakula na kuku kwa matumaini ya kupata faida kutokana na uwekezaji huu. Kwa kawaida mwanzoni kila kitu huonekana kwenda vizuri mpaka pale mfugaji anaposhtushwa na milipuko ya magonjwa ambayo hupunguza uzalishaji wake na hata kuua ndege wake wa thamani.
Mfugaji huyu afanye nini ili aweze kuepuka hasara hizi?. Uzoefu wa ulimwenguni kote unaonyesha kwamba kuweka mabanda, chakula na maji katika mazingira ya usafi ndio jambo la msingi kuweza kudhibiti magonjwa ya mara kwa mara kama kikoti, kipindupindu cha kuku, kuharisha (typhoid) na mengineyo. Ili kuwa makini kwenye uzalishaji wa kuku inapasa pia mfugaji kuzingatia chanjo dhidi ya majanga ya magonjwa kama vile kideri na ndui ya kuku.
*DONDOO ZA KUJILINDA NA MAGONJWA USIMAMIZI MZURI WA MABANDA YA KUKU*
• Banda la kuku linatakiwa kuwa safi na kavu wakati wote
• Banda la kuku lazima lipitishe hewa kwa wingi na kwa urahisi (well ventilated) na epuka joto kali na unyevunyevu kupita kiasi ndani ya banda la kuku.
• Ondosha vinyesi na takataka ndani ya banda mara kwa mara. Vinyesi (samadi) hutupatia mbolea yenye wingi wa madini ya fasifarasi na
naitrojeni.
• Safisha banda mara linapokuwa limechafuka, pulizia viuatilifu (disinfenctants) kama V-rid mara kwa mara na ubadilishe matandazo ndani
ya banda mara kwa mara.
• Jenga vichanja (perches), matundu ya kutagia, vyombo vya kutosha vya maji na chakula na sehemu ya vumbi kwa ajili ya kuku kujisugulia
(dust bathing).
• Dhibiti panya wa jamii za panya zisiweze kuingia ndani ya banda na kwenye ghala la chakula kwani hubeba (carriers) viini vya ugonjwa.
*USIMAMIZI BORA WA KUKU
*
• Wape kuku wako chanjo dhidi ya magonjwa hatari kama inavyoshauriwa na bwana mifugo, chanjo huanza kutolewa katika juma la mwanzo kama vile dhidi ya ugonjwa wa kideri na kuweza kurudiwa baadaye
• Usiwaweke kuku wengi pamoja kwa sababu iwapo kuku watalundikana kutapelekea uwezekano wa kutokea milipuko na maambukizi
ya magonjwa.
• Watenge vifaranga kutoka kuku wakubwa(isipokuwa wale waliokuwa na mama yao) kwa sababu ni rahisi kwa vifaranga kuambukizwa magonjwa.
• Weka uzio wa nje ya banda na wahamishe toka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya banda mara kwa mara.
*USIMAMIZI MZURI WA CHAKULA*
• Wapatie kuku wako mlo kamili na kwa kiwango kinachowatosheleza na uwape nyongeza ya chakula kama vya majani, mifupa na magamba ya mayai.
• Hakikisha unawapatia maji safi wakati wote
• Safisha malishio na manywesheo kila siku hakikisha unayasugua na kusuuza vilivyo ili kuondoka utando unaoota kwa sehemu za ndani
ambazo kwa kawaida huhifadhi vijidudu hatarivya bakteria kama Salmonella na E. coli.
• Nunua chakula chako kutoka msambazaji aliyethibitisha ili kuepuka uwezekano wa kuuziwa chakula kulichochafuliwa na sumu kuvu za Aflatoxin au salmonella na nyinginezo.
• Hifadhi chakula cha kuku kwenye sehemu kavu na baridi na usiache chakula ghalani zaidi ya miezi 3 kuepuka uwezekano wa kuzalisha sumu kuvu.
• Usilishe kuku wako chakula chochote ambacho kimeanza kutoa harufu ya uvundo au ukungu
*UDHIBITI WA MAGONJWA*
• Pata ushauri wa mtaalamu wa mifugo mara tu utapoona dalili za mwanzo za ugonjwa kwenye banda la kuku. Watenge kuku wagonjwa na waanze kuwatibu mara moja au ikibidi wateketeze ili kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa.
• Waondoshe haraka kuku waliokufa na wafukie shimoni au wateketeze kwa moto, na usijaribu kuwala kuku wagonjwa kwani kuna magonjwa huweza kuathiri hata binaadamu iwapo atawala kuku walioathiriwa na magonjwa.
• Iwapo itatokea milipuko ya magonjwa sehemu husika basi inakupasa kutoruhusu wageni kuingia bandani kwani watu huweza kusambaza magonjwa kupitia viatu, nguo wanazovaa na mikono, vilevile magari yanaweza kuingiza vijidudu vya magonjwa kupitia matairi, majukwaa ya kushushia mizigo na sehemu za chini za gari za kuhifadhia mizigo.
0 Comments